Waweza Kuishi na Yesu, lakini huwezi kuishi bila Yesu.Yohan 3:16



NI JINSI GANI MUNGU ANAHITAJI

TUMUIMBIE?

  • Je biblia humaanisha nini isemapo "tumsifu Mungu kwa matari  na kucheza (zaburi 150:4)?
  • Je biblia humaanisha nini izungumziapo kucheza?
  • Vipi kuhusu wakristo waimbao kwa kucheza, je wanafuata kile Biblia isemacho au wamepotoshwa?
  • Ni kanuni gani za kuzingatia ili tuimbe nyimbo zikubalikazo mbele za Mungu?
  • Je uimbaji ulianza lini katika Biblia?
  • Biblia hutoa muongozo gani kuhusu matumizi ya vyombo vya muziki?
  • Kuna usahihi wowote kuwakataza watu wasicheze katika Ibada wakati biblia humuonyesha daudi na wakati Miriam akicheza?  

Majibu ya aswali haya na mengine mengi yahusuyo mziki waweza kuyapata katika somo hili, fuatiliasomo hili kwa makini mpaka mwisho na Bwana atakufunulia siri ya pekee sana juu ya muziki ukubalikao mbele zake kwa mujibiu wa Biblia.

Uimbaji ni mojawapo ya huduma takatifu zinazoendeshwa katika ibada au mikutano ambapo watu hukusanyika ili kumwabudu Mungu Mwenyenzi aliye mkuu na muumbaji wa vitu vyote vilivyo hai na visivyo hai hapa duniani na mbinguni. Mungu mwenyewe ametoa miongozo ndani ya neno lake takatifu ni jinsi gani watu waenende mbele zake wakati wa ibada. Miongozo hiyo inapaswa iangaliwe na kufuatwa kwa makini sana ili ibada iweze kupata kibali machoni pa Mungu na hao waabuduo waweze kupata kibali machoni pake vile vile na Baraka tele. Ibada ni tendo(worship is a verb).

Ibada kamili lazima iwe na mambo
1.      Lazima tujiandae kuabudu
2.      Tujiandae kusikia neno la Mungu
3.      Kujiandaa kuitikia kile Mungu anacho tuambia na
4.      Kukubali kutumwa na Mungu
“Katika mambo hayo humaanisha kuwa, ibada ni tendo la kumwabudu na kumsifu Mungu;katika ibada Mungu sharti anenenasi na kutenda nasi;katika ibada huitkia sauti ya Mungu na kuhudumiana na viumbe wote vyote hujumuika jamopa katika ibada”Robert W.Webber uk26

 Sababu za Kuimba

Je, umewahi kuketi chini na kutafakari walao kwa muda wa nusu saa ukitafakari kwa nini unaimba nyimbo za dini? Mtu, kwaya au kikundi chochote cha uimbaji, kama hawaelewi sababu ya kutunga na kuimba nyimbo zao, basi ni rahisi sana kuifanya huduma kwa mtazamo na malengo yote ya uimbaji kinyume na mapezi ya Mungu. Ikumbukwe kwamba ‘katika muziki wa kidini Mungu ndiye kiini, na sio mambo ya ubinafsi wa mtu. Wazo la kumsifu Mungu kwa ajili ya kujiburudisha ni wazo geni katika Biblia.’[1] Vile vile kufanya huduma ya nyimbo kwa madhumini ya kujipatia fedha ni mawazo potovu yayoiharibu sana huduma hii takatifu sana.
Mfanyieni Bwana kelele za shangwe

Hindu ya rejea kwa sauti kubwa ya muziki inatukumbusha kuhusu onyo, “mfanyieni Bwana kelele za shangwe.” Usemi unajitokeza mara kwa mara katika Biblia ya tafsri ya mfalme James (KJV) lakini kwa tofauti kidogo katika Agano la Kale (Zaburi 66:1; 81:1; 95:1-2; 98:4, 6; 100:1). Mafungu haya ya Biblia yametumiwa mara kwa mara kutetea matumizi ya sauti ya juu  katika muziki wa ‘rock’ (aina ya dansi ya kurukaruka ndani ya kanisa). Man‘ruwa,’-רוע  Neno hili halimaanishi kufanya kelele za juu zisizochaguliwa kwa busara, bali ni kupaza sauti kwa furaha… mfano mzuri unapatikana katika kitabu cha Ayubu 38:7 mahali ambapo neno lilo hilo ruwa’-רוע
limetumiwa kuelezea wana wa Mungu ‘walipopaaza sauti kwa furaha’ baada ya umbaji. Uimbaji wa viumbe vya mbinguni wakati wa uumbaji hauwezi kabisa kuelezewa kuwa ni kelele za juu kwa sababu kelele huashiria sauti mbaya.’[2]

Mara nyingi watu wa Mungu wamekosa mibaraka yake kwa sababu ya vurugu nyingi na ambazo hazina maana yoyote wanapokuwa mbele za Mungu kwa ajili ya kumwabudu. Uwepo wa Mungu unakosekana. Ibada na hasa katika uibaji wa kwaya hugeuka kuwa maburudisho yenye mvuto wa kidunia.  Hivyo baraka za Mungu zinakosekana. Watu hurudi nyumbani kama walivyokuja na pengine hurudi nyumbani wakiwa wamechanganyikiwa zaidi ya walivyokuwa walipokuwa wakija kwenye ibada. Mungu hawezi kubariki fujo na machafuko hata siku moja. Kwa maana ‘Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani; vile vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu.’ (1Wakorintho 14:33). Kwa sababu hiyo mashauri yametolewa kwamba ‘Lakini mambo yote na yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu (1Wakorintho 14:40).
Ni jambo la muhimu sana kwa wote waabuduo kukumbuka daima kuwa kama kuna jambo nyeti na lenye uzito wa pekee ni lile la kwenda kukutana na Mungu katika ibada. Kicho na adabu halisi vinapaswa kuonekana katika maisha ya waabuduo. Sababu ni kwamba  Mfalme Mkuu, ndiyo Mungu mwenye nguvu, Muumbaji wa mbingu na nchi na vyote vilivyomo, Mwokozi wetu wa pekee Yesu Kristo, kwa njia ya Roho wake Mtakatifu anakuwa na watu wake katika ibada. Nao malaika kutoka mbinguni mahali ambapo uzuri na utaratibu kamili hutawala mile na hata milele, hujihudhurisha katika mikutano ya watu wa Mungu wakutanapo ili kutoa sifa na kumwabudu Mfalme wa milele au kufanya jambo lolote lile kwa ajili yake

Kwanza kabisa tunaona katika maandiko matakatifu habari ya wanawake wakicheza kwa mara ya kwanza katika kutoka 15:20, 21. ‘Na Miriamu, nabii mke, ndugu yake Haruni, akatwaa tari mkononi mwake; wanawake wakatoka wote wakaenda nyuma yake, wenye matari na kucheza. Miriamu akawaitikia mwimbieni Bwana, kwa maana ametukuka sana; farasi na mpanda farasi amewatupa baharini.’ Tukio hili lilitokea baada ya Mungu kuwaangamiza Wamisri kwa kuwafunika na maji katika bahari ya Shamu wakiwa katika harakati za kuwafuatia Wana wa Israeli ili kuwarudisha utumwani katika nchi ya Misri. Tunaambiwa kuwa Miriamu pamoja na wanawake wengine walicheza. 

Neno la Kiebrania lililotumika hapa ni miholah’ (מְחֹלָה) ambalo humaanisha kutembea katika mduara. Biblia, tafsiri ya KJV hutafsiri ‘dansi’ ya muduara. Lakini maana yake halisi ni kutembea (matching) katika mduara. Kwa kufafanua zaidi, miholah’-מְחֹלָה    humaanisha kucheza (kutembea)  katika mistari miwili, kucheza katika kambi la jeshi.’ Mara nyingi hueleweka kwamba jeshi au askari wanacheza gwaride. Jeshi Lichezapo gwaride halinengui bali hutembe katika mwendo maalum ambao hupangiliwa katika mistari miwili au zaid,mwendo huu huwa katika utaratibu uliokubalkikai. Hivyo wanawake waliomfuata Miriamu nyuma walikuwa wakienda kwa kumachi (kutembea) na sio kwa kukatika, kurukaruka au kunengua viuno vyao. Kutafsiri fungu hili kumaanisha kwamba ilikuwa ni ‘dansi’ ya kukatika au kunengua viuno ni kulitendea isivyo halali fungu hili la Biblia. Jambo lingine la kuzingatia katika tukio hili la Miriamu na wanawake wenzake ni kwamba hawakuwa kwenye mkutano wa ibada au mkutano wowote wa mafundisho ya neno la Mungu. Bali walikuwa safarini kutoka katika nchi ya Misri kwenda Kanaani na walikuwa jangwani.

Kwa upande mwingine neno hilo hilo ‘miholaמְחֹלָה limetumiwa katika 1Samweli 18:6 ambapo tunasoma, ‘hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda.’ Katika Waamuzi 11:34, hapo napo neno ‘mihola’מְחֹלָה limetumiwa wakati binti wa Yeftha alipotoka kumlaki baba yake alipotoka vitani. Matukio yote hayo hayawezi kuchukuliwa kama kigezo cha Wakristo kuimba na kucheza dansi katika mikutano ya ibada. Matukio hayo hayakuwa ya ibada. Katika matukio yote hayo wanaoonekana wakicheza ni wanawake peke yao. Siku hizi wanaume katika kwaya mbalimbali wanaonekana wakicheza na kurukaruka kama wendawazimu.

Katika 2Samueli 6:14 Mfalme Daudi aliopkuwa analileta sanduku la agano katika mji wa Daudi, yeye alicheza mbele za Bwana kwa nguvu zake zote. Neno la Kiebrania lililotumika hapo ni kara’  כָּרַר  ambalo humaanisha kurukaruka na kuzungukazunguka (leaping and whirling) na wengine hufasiri kucheza. Hivyo maana yake halisi ni kwamba, kwanza Daudi alikuwa kwenye msafara wa kulileta sanduku la Bwana kutoka kwenye nyumba ya Obed-Edom hadi kwenye mji wa Daudi. Akiwa kwenye msafara huo, Daudi, kwa furaha kubwa alionekana akirukaruka na kuzunguka zunguka mbele ya sanduku la Bwana.

Mambo ya kuzingatiakatika muktadha wa uchezaji wa Daudi:
1.      Daudi hakuwa na maandalizi yoyote ya namna ya kucheza. Yeye alizunguka zunguka huko na huko na kuruka kuruka huko na huko jambo ambalo mtu yeyote anaweza kulifanya apatwapo na furaha isiyo na kifani. Mfano mzuri ni pale mtoto apatapo matokeo ya mtihani na kuona kuwa amefauru kwa kiwango cha juu sana. Anaweza kuruka ruka na kucheza cheza bila ya maandalizi yoyote ni jinsi gani angeruka ruka endapo angefauru vizuri. Na kucheza kwa Daudi kulikuwa ni tukio la papo hapo. Halikuwa tukio la kuendelea au mtindo wa ibada ya uimbaji.
2.      Hakuwa na timu au kikundi cha watu ambacho alifanya nacho maandalizi kwa ajili ya kucheza.
3.      Hakuwa Hekaluni au kwenye mkutano wa ibada au mafundisho yoyote ya neno la Mungu. Alijua wazi kwamba ndani ya nyumba ya ibada hakuna kurukaruka au kuzunguka zunguka kwa namna iwayo yote maana imeandikwa, ‘Lakini Bwana yumo ndani ya hekalu lake takatifu; dunia yote na inyamaze kimya mbele zake (Habakuki 2:20).
4.      Daudi hakuwa anacheza kama ni sehemu ya ibada mbele za Mungu aliye hai. Pia hatuoni kama alikuwa anaimba wimbo wowote wakati alipokuwa anarukaruka na kuzunguka zunguka mbele ya sanduku la Bwana. Wala haikuwepo kwaya yoyote ikiimba nyimbo. Kurukaruka na kuzunguka zunguka kwa Daudi mbele ya sanduku la Bwana au Miriamu  pamoja na wanawake waliomfuata nyuma, hakuwezi kuchuliwa kuwa ni kigezo cha kuhalalisha dansi katika kanisa la Mungu aliye hai au katika ulimwengu wa Kikrsito.

Katika Zaburi 149:3 na 150:4, kuna neno jingine la Kiebrania linalofasiriwa kama ‘dansi’ ambalo ni ‘maholi’- מָחוֹל . Haya mafungu ya Biblia ni ya muhimu sana kwasababu Ibilisi na makanisa yachezayo dansi huyatumia kuunga mkono hoja ya watu wengi kuwa ‘dansi’ ni sehemu ya ibada kanisani. Ikiangaliwa kwa makini sana itaonekana kuwa neno ‘dansi’ katika mafungu haya mawili ya Biblia linabishaniwa sana na wana-eliungu (Theologians). Baadhi ya wana-eliungu huamini kwamba ‘maholi’-מָחוֹל  hutokana na neno ‘chuwl’ amabalo humaanisha ‘fanya uwazi.’ Kwa maelezo hayo inawezekana ni chombo cha muziki chenye uwazi kama vile bomba. Tafsiri hii yaweza kuwa sahihi kwa sababu ukiangalia kwa makini sana, tunaweza kuona kuwa ‘maholi’-מָחוֹל  ni chombo cha muziki kwa sababu katika  Zaburi 149:3 na 150:4 kuna mlolongo wa vyombo vya muziki kama ifuatavyo:

Zaburi 150:3- Kwa mvumo wa baragumu……kwa kinanda na kinubi
             150:4-kwa matari   na kucheza (maholi)-מָחוֹל
             150:4-Kwa zeze     na    filimbi
             150:5- Kwa matoazi yaliyao………kwa matoazi yavumayo

Katika sura hii sehemu zote za mafungu kuna usambamba (parallelism) wa vyombo vya muziki tu isipokuwa chombo cha muziki ‘matari’ ndiyo huambatanishwa na kucheza. Msambamba wa vyomvo vya muziki katika sura hii ni wazi kuwa neno lililofasiriwa kama ‘kucheza’ kutoka katika neno la Kiebrania ‘maholi’-מָחוֹל  si sahihi. Neno ‘maholi’-מָחוֹל  linaonekana kuwa chombo cha muziki katika Zaburi 149:3 na Zaburi 150:4. Neno hilo linatokea katika mlolongo wa vyombo vinavyoweza kutumika katika kumsifu Bwana. Kwa kuwa mtunga zaburi anaoorodhesha vyombo vyote vinavyoweza kutumiwa katika kumsifu Bwana ni vyema kuelewa kuwa ‘maholi’- מָחוֹל  ni chombo cha muziki, kwa namna yoyote kinavyoweza kuonekana.[3]

Katika Muongozo wa ‘The Study Bible,’ tafsiri ya Mfalme James, katika ‘footnote,’ inatafsiri neno ‘maholi” מָחוֹל kuwa ni chombo cha muziki aina ya ‘bomba’ (pipe).[4] Zamani, katika shule za msingi, bendi za shule zilikuwa na wapiga filimbi ambazo zilikuwa ni bomba refu kidogo na matundu kama matano au sita . Ngoma ilipopigwa na wapiga filimbi walipiga muziki kusindikiza mlio wa ngoma. Chombo cha jinsi kama hiyo hiyo chaweza kutumika katika kumsifu Mungu. Izingatiwe kwamba, ‘neno la Kiebrania lilofasiriwa “Zaburi” linatokana na neno la asili linalomaanisha ‘kuimba kwa kutumia vyombo vya muziki.’[5] Katika Zaburi 81:2 tunasoma, ‘pazeeni Zaburi (vyombo vya muziki), pigeni matari, kinubi chenye sauti nzuri, na kinanda.’ Hapa anataja kupaza Zaburi ambayo humaanisha chombo chochote kinachoweza kutumiwa katika kumsifu Mungu. Kwa hiyo dhana ya kwamba Zaburi 150:4 huelekeza watu kucheza dansi mbele za Mungu ni dhana potofu na tafsiri iliyopotoka.

Bila shaka watu wengi wanaweza kuibuka na hoja kwamba, ni kweli ‘maholi’-מָחוֹל   chaweza  kuwa ni chombo cha aina fulani cha muziki na hasa chombo cha muziki abamcho ni kama aina ya bomba (pipe); lakini je mfalme Daudi hakuwahi kucheza mbele za Bwana Mungu? Jibu liko wazi kabisa. Ni kweli aliwahi kucheza. Neno la Kiebrania ‘karar’-כָּרַר  lililotumika katika 2Samweli 6:14 kama tulivyoona hapo awali, humaanisha kurukaruka na kuzunguka zunguka. Davidson anaeleza karar’-כָּרַר  kuwa ni kurukaruka. Pia kwamba mwana-kondoo anaitwa hivyo (karar) kwa sababu ya kurukaruka kwake.’[6]

Maana halisi ya neno kucheza katika Biblia
Kwa wale wote wenye dhana potofu kwamba Daudi alicheza dansi katika 2Sameli 6:14 ;Zaburi 149:3 na 150:4 anasistiza kwamba watu wamwimbie Bwana kwa matari na kucheza, wanapaswa kuelewa kuwa :
  • Katika 2Samweli 6:14 neno la Kiebrania lilotumika ni ‘karar’- כָּרַר  humaanisha kurukaruka na kuzunguka zunguka.
  • Katika Zaburi 149:3 na 150:4 neno la Kiebrania lilotumika ni ‘maholi’ -מָחוֹל  humaanisha chombo cha muziki cha aina kama ya bomba (pipe). Maneno haya yana maana tofauti na vile watu waelewavyo kuwa ni uchezaji dansi
  • Daudi hakucheza dansi katika 2Samweli 6:14 bali ali-‘karar’-כָּרַר   yaani alirukaruka kama mwana-kondoo aliyenenepeshwa anavyorukaruka akiwa nje ya zizi. Na wala hakuwa ana- ‘maholi,’- מָחוֹל  yaani akipiga chombo cha muziki. Mwana-kondoo huwa hana maandalizi au mafunzo ni namna gani arukeruke. Mwana-kondoo anarukaruka bila ya kufuata mwelekeo wa aina fulani na wala hafuati mapigo au mudundo fulani. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Daudi. Hakuwa na muda wa kujifunza na wala hatuambiwi ya kwamba aliwahi kwenda kwenye shule yoyote ya kujifunza namna ya kucheza mbele za Bwana kwa ustadi wa mwelekeo fulani kama kwaya nyingi zifanyavyo siku hizi.
  • Daudi hakujikaririsha njia iwayo yote ile kwa ajili ya kurukaruka na kutupa mikono na miguu huko na huko kama kwaya za leo zifanyavyo kwa kushinda ndani ya jengo la kanisa au kwenye viwanja fulani na kujikaririsha ni namna gani wataruka kwa pamoja na kutupa mikono kwa pamoja. Na ieleweke tu kwamba kwaya za siku hizi hazipo kumwimbia na kumsifu Mungu bali zipo kwa ajili ya kutimiza kiu yao kali ya dansi ya dunia huku wakiwa wameivika dansi yao vazi la Kikrsito. Kwa lugha rahisi, kile kinachofanywa na kwaya za siku hizi ni ‘upagani mambo kikristo.’ Kwa upande mwingine lazima tukubali kuwa pepo mchafu ameingia katika fani ya uimbaji na muziki kwa ujumla na ni lazima akemewe kwa nguvu zote ili atoke katika mioyo ya waimbaji ili wabaki wakimwimbia Bwana na kumtukuza yeye tu.

Mashauri ya nabii Ellen G white kuhusu uimbaji
Makelele na midundo na kucheza ni ishara ya ukaribu wa kufungwa kwa mlango wa rehema . Mjumbe wa Mungu anaelezea kile ambacho Bwana alimwonyesha kuhusu ibada ya ghasia na makele ambazo huonekana katika ibada siku hizi.

‘Mambo yale umeyaelezea…Bwana amenionyesha kwamba yatatokea tena kabla ya kufungwa kwa mlango wa rehema. Kutakuwepo na kupiga makelele, pamoja na ngoma, muziki, na kucheza. Akili za mwanadmu zitachanganyikiwa kiasi cha kwamba hazitaweza kuaminiwa kufanya maamuzi sahihi.’[7]

White pia anasema kuwa, ‘Bwana amenionyesha kwamba nadharia na mbinu potovu vitaingizwa katika makambi yetu, na kwamba historia ya zamani itarudiwa…Mambo yale yaliyokuweko wakati wa nyuma yatakuwepo siku za mbele (ndio sasa). Shetani ataufanya muziki kuwa mtego kwa namna unavyoendeshwa. Mungu anawaita watu wake, amabao wana ushuhuda, kusoma na kutafakari kwa makini, na kuchukua jukumu la kusikia.’[8]

Ni muhimu kwa watu wa Mungu kuelewa kuwa uimbaji wajinsi hiyo kamwe hauongozwi na uwezo wa Mungu Roho Mtakatifu. Mjumbe wa Mungu anasema tena kwamba, ‘Roho Mtakatifu kamwe hajidhihirishi mwenyewe kwa njia kama hii, katika ghasia za makelele. Huu ni ubunifu wa shetani ili kufunika werevu wa mbinu zake ili kuufanya ukweli ulio safi, ulionyoka, wenye kuinua, wenye kunfanya mtu kuwa mungwana, ukweli wenye kutakasa kwa wakati huu usiwe na matokeo mazuri. Ni vema kutokuwa na ibada ya Mungu iliyochanganywa na muziki kuliko kutumia vyombo vya muziki kufanya kazi ambayo mnao January lilionyesha kwangu kwamba italetwa katika makambi yetu…Ghasia za makelele hushitua akili na hupotosha kile ambacho kama kingeendeshwa vizuri kingeweza kuwa Baraka…Mambo yote yaliyokuwepo siku za nyuma yatajitokeza siku za usoni. Shetani ataufanaya muziki kuwa mtego kwa jinsi uanvyoendeshwa.’[9]

Kucheza, midundo ya muziki na midundo ya ngoma na kadhalika vimetawala na kuwa chanzo cha machafuko katika ibada.
Mjumbe wa Mungu anasema kuwa,
 ‘Roho Mtakatifu hana sehemu yoyote katika makelele na milio mikubwa kama ilivyopita mbele zangu… Shetani anafanya kazi katika makelele na machafuko ya muziki, ambao kama uingefanywa kwa usahihi, ungekuwa ni sifa na utukufu kwa Mungu. Anafanya madhara ya       huo muziki kama sumu kali ya nyoka.’[10]
Naliona ya kwamba utaratibu wa Mungu umebadilishwa, na miongozo yake muhimu imepuuzwa na wale wote wanaoiga utamaduni wa Amerika. Nilirejeshwa kwa fungu la Kumbukumbu la Torati 22:5 kwamba mwanamke asivae mavazi yampasyo mwanamume…kumekuwapo na hali ya wanawake katika mavazi yao na mwonekano wao kuwa karibu sana sawa na ule wa wanaume kwa kadiri iwezekanavyo, na wanashona mavazi yao karibu sana na yale ya wanaume, lakini Mungu anasema wazi kuwa hayo ni machukizo.’[11] 1T 457
Wakati kanisa zima au kwaya maalumu inapoimba nyimbo za kumsifu na kumtukuza Mungu Aliye Mkuu kwa kuimba kwa uzuri , utaratibu na utakatifu wote, malaika nao huunganika nao katika kumsifu Mungu huku wakivipiga vinubi vyao Mara nyingi, kwenye mikutano ya jinsi hiyo waabuduo wanatoka wakiwa wamepata burudiko la Kiroho na ‘ruwa,’-רוע  Neno hili halimaanishi kufanya kelele za juu zisizochaguliwa kwa busara, bali ni kupaaza sauti kwa furaha…
Katika kitabu cha Ayubu 38:7 mahali ambapo neno lilo hilo ‘ruwa’-רוע   limetumiwa kuelezea wana wa Mungu ‘walipopaaza sauti kwa furaha’ baada ya umbaji. Uimbaji wa viumbe vya mbinguni wakati wa uumbaji hauwezi kabisa kuelezewa kuwa ni kelele za juu kwa sababu kelele huashiria sauti mbaya.’[12]

Waimbaji wapaswa kuadabishwa
 E.G. White alikutana na tatizo hili siku za maisha yake na utumishi akasema  ‘lakini wakati mwingine ni vigumu zaidi kuwaadibisha waimbaji na kuwaweka katika utaratibu wa kazi…Wengi wanataka kufanya mambo kwa kufuata mtindo wao wenyewe; wanakataa kushauriwa; na hawako tayari kusikiliza uongozi.’[13]


Mahali na Wakati wa Kuimba

Biblia haituelekezi tu kuimba katika nyumba ya Mungu, bali pia miongoni mwa wasioamini, katika nchi za kigeni, na wakati wa mateso, na katikati ya watakatifu mwandishi wa kitabu cha Waebrania anasema, ‘nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu; katikati ya kanisa nitakuimbia sifa (Waebrania 2:12).

Mtunga Zaburi anasisitiza kwa kusema, ‘mwimbieni Bwna wimbo mpya, sifa zake katika kusanyiko la watauwa (Zaburi 149:1). 

Naye mtume Paulo imeandikwa, ‘kwa hiyo nitakushukuru kati ya mataifa, nami nitaliimbia jina lako (Warumi 15:9).

Katika kitabu cha nabii Isaya imeandikwa, ‘jangwa na miji yake na ipaze sauti zao, vijiji vinavyokalia na Kedari, na waimbe wenyeji wa Sela, wapige kelele toka vilele vya milima, na wamtukuze BWANA, na kutangaza sifa zake visiwani (Isaya 42:11, 12). 

Wakiwa gerezani, Paulo na Sila ‘walilkuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za sifa, na wafungwa wengine walikiuwa wakiwasikiliza (Matendo ya Mitume 16:25).

Kwa mafungu hayo machache ni wazi kuwa nyimbo za kumsifu Mungu zaweza kuimbwa popote pale. Gerezani, katikati ya mataifa, kanisani na katika kusanyiko lolote la watakatifu. Mwanadamu anaitwa kumwimbia na kumsifu Mungu mahali popote pale alipo. Kwamba ana furaha au huzuni, ana njaa au shibe na amwimbia na kumsifu Mungu Muumbaji.

Hindu za rejea za mara kwa mara kwa ajili ya kumsifu Mungu miongoni mwa wapagani au watu wa mataifa (2Samewli 22:50; Warumi 15:9; 108:3) huashiria kuwa uimbaji ulionekana kuwa njia ya kumshuhudia BWANA kwa watu wasioamini. Hata hivyo hakuna uthibitisho wowote katika Biblia kwamba Wayahudi au Wakristo wa kwanza walifuatisha sauti na nyimbo za kidunia ili kuweza kuwahubiri watu wa mataifa.

Wayahudi na Wakristo wa kwanza waliamini kuwa muziki wa kidunia ulikuwa hauna nafasi katika nyumba ya ibada.[14] 

Mwanzo wa Huduma ya Muziki Katika Biblia:
Kabla ya wana wa Israeli kuingia katika nchi ya Palestina, huduma ya muziki wakati wa ibada kwa kusudi la kukidhi mahitaji ya waabuduo haikuwepo. Kabla ya wakati huo hindu za rejea kwa muziki kimsingi zilihusiana na wanawake kuimba na kucheza kwa ajili ya kusherehekea tukio fulani maalumu. Mfano wa kwanza kabisa ni ule wa Miriamu akiongoza kundi la wanawake ambao walikuwa wakiimba na kucheza kwa sababu Bwana Mungu aliwatupa Wamisri katika bahari ya Shamu na kuwangamiza huku akiwaokoa wana wa Israeli kwa muujiza wa ajabu kabisa (Kutoka 15:1-2). Pia, wakati Daudi alipomua Goriathi ambaye alikuwa ni tishio kubwa kwa wana wa Israeli, wanawake walicheza wakishangilia ushindi huo mkuu (1Samuli 18:6-7). Na mfano mwingine ni ule wa binti wa Yefta ambaye alimlaki babaye kwa matari na kucheza aliporudi kutoka vitani (Waamuzi 11:34).

Jambo la kuzingatia hapa ni kwamba wote hao waliimba na kucheza wakati ambao sio wa ibada na nje ya mahali pakuabudia au kanisa/hekalu.  Kulingana na taarifa ipatikanayo katika kitabu cha Mambo ya Nyakati kitabu cha kwanza, mfalme Daudi alianzisha huduma ya uimbaji katika hatua tatu:
1.Aliagiza vichwa wa familia za Kilawi kuchagua watu wapigao vyombo vya muziki na kwaya kwa ajili ya kulisafirisha sanduku la Agano kutoka kwa Wafilisti hadi hemani kwake katika mji wa Yerusalemu (1Nyakati 15:16-24).
2.Hatua ya pili ilitokea wakati sanduku la Agano lilikuwa limewekwa katika hema lake katika mahali pake (1Nyakati 8:11), kwaya moja ilikuwa ikiimba chini ya uongozi wa Asafu mbele ya Sanduku la Agano katika Jerusalemu  (1Nyakati 16:37-42).
3.Hatua ya tatu ya uanzishaji wa huduma ya muziki ilitokea  mwishoni mwa utawala wa mfalme Daudi wakati mfalme alipoandaa kwa undani kabisa huduma ya muziki ambao ungetumika katika hekalu ambalo Sulemani angelijenga (1Nyakati 23:2 hadi 26:32). Daudi aliunda kundi la Walawi 4000 kuwa waimbaji wa pekee (1Nyakati 15:16; 23:5). Kutoka kwenye kundi hili mfalme Daudi aliunda kwaya ya Kilawi yenye waimbaji 288.

Daudi mwenyewe alihusika pamoja na maofisa katika kuchagua viongozi 24 kuwa walinzi, kila mmoja alikuwa na wanamuziki 12. Jumla yao ilikuwa ni wanamuziki 288 (Nyakati 25:1-7). Hao nao waliajibika katika kuchagua wanamuziki wengine.[15]
Huduma ya Wanamuziki
Ili kuhakikisha kuwa kusiwepo machafuko au mgongano kati ya huduma ya makuhani na huduma ya wanamuziki ya Walawi, mfalme Daudi, kwa uangalifu mkubwa sana alifafanua nafasi, cheo, na kusudi la huduma ya wanamuziki (1Nyakati 23:25-31). Utendaji wa huduma ya wanamuziki ulikuwa chini ya makuhani (1Nyakati 23:28).

Viongozi wa kwaya au walimu wa kwaya wanapaswa kuelewa fika utendaji wao ili kusiwepo mgogoro baina yao na wachungaji. Ukweli ni kwamba mchungaji ndiye kiongozi wa kwaya. Tatizo kubwa linalojitokeza katika kanisa ni lile la walimu wa kwaya kutaka kumtawala mchungaji na kutaka mchungaji akubaliane na kufuata matakwa yao hata kama yako kinyume na neno la Mungu au kanuni za kanisa. Walimu wa kwaya wengi hukanyaga chini taratibu za kanisa na kufanya mambo kama wapendavyo kwa ajili ya faida yao wenyewe na familia zao badala ya kufanya kazi ya uimbaji kwa ajili ya Mungu.

Walimu wengi sana wa kwaya wamejaa kiburi na ukaidi usio wa kawaida. Wanadharau neno la Mungu, wanadharau uongozi wa kanisa na taratibu zake zote. Roho hiyo hiyo inaingizwa kwa waimbaji wote ambao nao hawako tayari kuheshimu wazee wa kanisa na wachungaji. Wanadharau taratibu zote za kanisa. Kiongozi wa kwaya anageuka kuwa mungu wao. Hili halikuanza leo. Tangu zamani roho ya ukaidi na kiburi, ikianzia na shetani mwenyewe kule mbinguni, imeonekana katika maisha ya waimbaji.

 Mjumbe wa Mungu E.G. White alikutana na tatizo hili siku za maisha yake na utumishi na aliandika, ‘lakini wakati mwingine ni vigumu zaidi kuwaadibisha waimbaji na kuwaweka katika utaratibu wa kazi…Wengi wanataka kufanya mambo kwa kufuata mtindo wao wenyewe; wanakataa kushauriwa; na hawako tayari kusikiliza uongozi.’[16]

Hili ni tatizo kubwa ambalo huleta giza na laana isiyo ya kawaida katika kanisa la Mungu.
· Kwaya nyingi sana zinafanya maamuzi zenyewe ni namna gani wataimba ili kukidhi haja yao ya muziki wa kidunia ambayo wengi waliipata kabla ya kuingia kanisani.
· Kwaya haziko tayari kuwasikiliza wazee wa makanisa labda kama naye mzee awe ametekwa na kuingia katika ukafiri wa jinsi hiyo hiyo.
· Kwaya haziko tayari kusikiliza wachungaji na adui yao mkubwa ni Roho ya Unabii na Biblia kwa ujumla. Kwaya nyingi zimekuwa ni mashirika yanayojitegemea ndani ya kanisa. Na wanaofaidika na kile kinachotokana na uimbaji huo ni wachache sana. Wengine wanakuwa ni bendera fuata upepo. Pale uongozi unapojaribu kusahihisha na kerekebisha uimbaji wao, na wakiona mafundisho yanapingana na matakwa yao na maslahi yao kwa ujumla, utajionea mwenyewe roho ya uasi iliyo ndani yao. Ndipo utajua kuwa wamevaa ngozi ya kondoo lakini ndani ni mbwa mwitu wakali mno. Wako tayari kupigana, kutukana na kubeza uongozi. Kweli hata ibilisi alipoona mambo yake yanapingwa kule mbinguni, aliazimia kupigana na roho hiyo hiyo imeipandikiza ndai ya waimbaji na hasa walimu wa kwaya walio wengi (Ufunuo 12:7-12). Ibilisi hakushinda kule mbinguni. Akatupwa chini. Kama Bwana aishivyo, waimbaji wote pamoja na walimu wao wanao kaidi neno la Mungu na kushindana na uongozi wa kanisa, muda si murefu watatupwa chini na wala hawatalishinda neno la Mungu.

VYOMBO VYA MUZIKI NA MATUMIZI YAKE KATIKA AGANO LA KALE NA JIPYA

Haiwezekani kuongelea habari ya vyombo vya muziki katka ulinasi wa Kikrisito siku hizi na upigaji wake katika ulinasi wa Kikrsito wa sasa bila ya kuchunguza katika Agano la Kale kama vilitumikaje. Kama tulivyokwisha kuona katika sura iliyotangulia, ‘Daudi hakuanzisha tu muda, mahali, na maneno kwa ajili ya huduma ya kwaya ya Walawi, lakini pia alitengeneza vyombo vya muziki ili vipate kutumiwa kwa ajili ya huduma yao.[17] Tunasoma, ‘na elfu nne walikuwa mabawabu; na elfu nne walimsiu BWANA kwa vinanda, nilivyovifanya, alisema Daudi, vya kumsifia (1Nyakati 23:5). ‘Wakasimama makuhani sawasawa na malinzi yao; Walawi nao pamoja na vinanda vya BWANA, alivyovifanya Daudi mfalme, ili kumshukuru BWANA, kwa maana fadhili zake ni za milele, hapo aliposifu Daudi kwa mikono yao; nao makuhani wakapiga panda mbele yao; nao Israeli wote wakasimama (2Nyakati 7:6). Hii ndiyo sababu inayofanya viitwe vyomb vya Daudi (2Nyakati 29:26-27).

Kwa mapanda ambayo Bwana aliyaamuru kupitia Musa, Daudi aliongeza matoazi, vinubi na vinanda (1Nyakati 15:16; 16:5-6). Mapanda yalipigwa na makuhani na idadi yao ilianzia mawili katika ibada ya kila siku (1Nyakati 16:6; Hesabu 10:2) hadi saba au zaidi wakati wa matukio maalumu (1Nyakati 15:24; Nehemia 12:33-35; 2Nyakati 5:12).

 ‘Wakati wa ibada pale Hekaluni mapanda yaliaashiria kusanyiko la waabuduo kusujudu wakati wa kutoa sadaka ya kuteketezwa na wakati wa kuitikia (Choral service) huduma ikiendelea (2Nyakati 5:12; 7:6).’[18]

 
“Mpangilio huu ulionyesha umuhimu wa wapiga mapanda kutoa ishara kwa ajili ya mkutano kusujudu na kwaya kuimba.[19]
‘Vyombo vya nyuzi vilitumika sana kusindikiza uimbaji kwani vilikuwa havifuniki sauti au maneno ya Yehova yaliyokuwa yakiimbwa.’[20] Uangalifu mwingi ulifanyika ili kuhakikisha kwamba sauti za sifa za kwaya hazikufunikwa na sauti za vyombo vya muziki.[21]

Kusudi hilo hilo la vyombo kusindikiza sauti za waimbaji linapaswa kufuatwa kwa makini leo. Lakini kwa bahati mbaya tena kwa makusudi kabisa vyombo vinapigwa na watu wasio na ujuuzi kabisa kwa sauti ya juu sana na midundo mizito na kufunika sauti za maneno ya sifa zinazotolewa na waimbaji hazisikiki na wala kueleweka. Badala ya waabuduo kutoka katika ibada na Baraka na kicho mbele za Mungu, wanatoka na vichwa vinavyouma na masikio yanayonyita kwa sababu ya midundo na kelele za juu sana za vyombo vya muziki tena vinavyopigwa bila utaratibu wala kicho mbele za Mungu.

Swali linaweza kuulizwa, ‘je tupunguze sauti za vyombo ili midundo isikike kwa chini kabisa? Jibu liko wazi kabisa. Sumu ni sumu tu. Kwamba iko kwenye pipa la lita 100 au ipunguzwe hadi kuwa katika nusu ya kijiko cha chai uwezo wake wa kufiisha uko pale pale. Kama mtu haelewi hata hilo basi na aelewe kwamba kinyesi ni kinyesi tu. Kwamba kimechotwa chooni na kuwekwa na kujazwa kwenye debe au kimewekwa kwenye kijiko cha chai madhara yake ni yale yale. Hivyo ndivyo ulivyo muziki wa midundo. Kwamaba imepigwa kwa sauti ya chini au ya juu madhara yake ni yale yale. Mungu haitaki kwa sababu inafiisha hali ya mtu kuyaelewa na kuyapokea mambo ya kiroho. Inalewesha wale ambao huipenda kiasi cha kwamba hawako tayari kusikia ushauri wowote utokao kwenye neno la Mungu na Roho ya unabii. Inapumbaza na kuilaza akili hata isitamani mafundisho yatokayo kwenye neno la Mungu.
Na izingatiwe kuwa ‘kamwe hakukuwa na vyombo vyovyote vya midundo vilivyoweza kuruhusiwa kusindikiza nyimbo za kwaya ya Walawi ilipokuwa ikitoa huduma ya nyimbo Hekaluni au kundi kubwa la wapiga muziki pamoja (Orchestra) pale Hekaluni (Ezra 3:10; Nehemia 12:27, 36). Waimbaji na vyombo vya muziki pale Hekaluni vilikuwa tofauti kabisa na vile vilivyotumiwa katika maisha ya kila siku ya watu.[22]

Kupitia fani ya muziki, laana na giza limeingia kanisani. Katika ibada nyingi malaika wa Mungu huwa wanaamua kuondoka pindi wanapoona nyimbo za zisizofaa na muzuki wa usiofaa unapoanza kupigwa.

 Mjumbe wa Mungu White anasema:
Mambo ya milele yana uzito kidogo sana kwa vijana. Malaika wa Mungu wanatoa machozi wanapoandika maneno na matendo ya Mkrisito. Malaika wanazunguka zunguka huko na huko. Vijana wamekutanika pamoja, kuna mlio wa sauti na vyombo vya muziki. Wakrisito wamekusanyika hapo, lakini ni nini unachokisikia? Ni wimbo, wimbo wa upuuzi, ufao katika ukumbi wa dansi. Tazama malaika wanaiondoa nuru kutoka kwao, na giza nene linawagubika wote walio katika eneo hilo. Malaika wanaondoka kutoka kwenye tukio hilo. Huzuni ijuu ya nyuso zao. Tazama, wanalia. Hili nililiona likirudiwa mara nyingi katika makundi yote ya watunzao Sabato…muziki ni sanamu ambayo wengi wa Wakrisito wa wanaokiri kuitunza Sabato. Shetani hana kipingamizi kwa muziki kama anaweza kuufanya kuwa njia ya kuyafikia mawazo ya vijana…Vijana wanakutana kuimba, na ingawaje wanakiri kuwa ni Wakristo, mara kwa mara wanamvujia Mungu heshima na imani yao kwa mazungumuzo ya upuuzi na uchaguzi wao wa muziki.[23]

Midundo ya muziki wa lege, jazz, rock za aina zote, na mingineyo, pale tu inapoanza kupigwa, malaika wa Mungu hawabaki hapo tena. Wanaondoka mara moja kwenye mkutano huo. Ni mkutano wa laana huo. Na malaika wa Mungu wakiondoka, mara moja shetani na malaika zake huja na kuchukua nafasi na kuongoza mkutano huo.

Nuru ya Mungu huondolewa kwenye mkutano huo. Giza nene huwafunika hao waliokusanyika kwa ibada mahali hapo. Badala ya kuwa mkutano wa Baraka unageuka kuwa mkutano wa laana kubwa ajabu. Rubani wa mikutano hiyo anakuwa ni ibilisi yule nyoka wa zamani. Je, hapo mahali ambapo ibilisi anongoza, unategemea waimbaji na wapiga vyombo na hasa keyboard wataitikia maonyo yoyote? Kamwe hawawezi kusikia maana roho mchafu wa shetani anakuwa ametawala na kuongoza mkutano huo. Jua wazi kwamba kabla hata malaika wa Mungu hawajaoondoka, Roho Mtakatifu anakuwa amekwisha ondoka zamani. Pepo mchafu anakuwa ametawala mkutano au ibada hiyo asili mia moja. Kwa sababu hiyo kanisa zima linakuwa chini ya chuki ya Mungu kwa sababu tu ya hao wachache ambao wamekataa neno la Mungu bali hufuata mapenzi yao.
Mungu anawaita watu wake kuwa watulivu na wenye msimamo. Wanapaswa kuwa waangalifu sana wasije wakamwakilisha vibaya na kuyavunjia heshima mafundisho makuu ya ukweli kwa njia ya maonyesho ya kigeni, kwa machafuko na makelele. Kwa haya, wale wasioamini wataongozwa kufikiri kuwa Waadventista wa Sabato ni kikundi cha ulokole…wakati waumini wanapohubiri ukweli kama ulivyo katika Yesu, wanadhihirisha utakatifu, utulivu, na sio dhoruba ya machafuko.[24]
Wote tunajua kuwa uimbaji wa kilokole ni wa midundo ya ngoma, kucheza na kurukaruka na sauti ya makelele ya juu sana. Kuna hitaji kubwa kwa mtu yeyote anayeijua kweli kusimama na kukemea uimbaji huu ambao ibilisi ameuingiza katika kanisa la Mungu kwa makusudi ya kuwapoteza watu Mungu yamkini hata walio wateule.
Ulokole, mara unapokuwa umeanza na kuachwa bila ya kuzuiwa, ni vigumu kuuzima kama vile moto ambao tayari unakuwa umeanza kuteketeza nyumba. Wote ambao wameingia katika hali ya ulokole na kukuubali huu ulokole, ni vyema sana waingie katika kazi za kidunia; kwa maana kwa mwelekeo huu wa matendo yasiyo sahihi wanamvunjia heshima Mungu na kuhatarisha watu wake. Mivuto mingi kama hii itainuka wakati huu, wakati ambapo kazi ya Bwana ingeinuliwa, iwe safi, bila ya kuchafuliwa na ushirikina na hadithi. Tunapaswa kuwa waangalifu, kudumisha uhusiano wa karibu pamoja na Kristo, ili kwamba tusidanganywe na shetani. Mungu anataka utaratibu na nidhamu katika huduma yake, sio msisimuko na machafuko. Kwa sasa hatuwezi kuelezea kwa usahaihi matukio ambayo yatatendeka katika ulimwengu wetu huu siku za usoni, lakini hiki ndicho tunachokijua, kwamba huu ndio wakati ambapo tunapaswa kukesha katika maombi; kwa maana siku kuu ya Bwana iko karibu sana. Shetani anaongeza nguvu zake. Tunapaswa kuwa watu makini na watulivu, na kutafakari kweli za ufunuo. Msisimuko haukubaliki kwa kukua katika neema, usafi wa kweli na utakaso wa roho.[25]

Dini ya kilokole imeuteka ulimwengu wa Kikristo na vile vile ulinasi wa kipagani. Sasa pia imeuteka ulimwengu wa Kikristo wa kanisa la Mungu la Waadvnetista wa Sabato. Ni wapi mtu ataweza kwenda asiweze kukutana na uimbaji wa midundo ya muziki na kucheza kwa namna ya kilokole? Nenda katika kanisa Katoliki ambalo miaka ya zamani lilisifika kuwa ma muziki wa dini hasa, nenda katika kanisa la Lutherani ambao walikuwa ni waimbaji mashughuli katika ulimwengu wa Kikristo, Moravian, Anglicana, na kadhalika, utakutana na muziki wa midundo na kucheza na kurukaruka.
 Nenda kweye virabu vya pombe kwamba ni vijijini au mijini utakutana na muziki wa midundo na kurukaruka iliyoimbwa na wale anaojidai kuwa ni Wakristo na ati wanamwimbia na kumchezea Yesu. Walevi waliisha acha miuziki ya wapigaji wa kidunia maana hao hawamdhihaki Yesu na wamegeukia muziki wa upagani mambo kikristo.
 Je, Roho ya Unabii inatoa maagizo gani katika fani ya uimbaji na muziki kwa ujumla?
    “‘Watu wengi, vijana kwa wazee, kwa maneno matamu wanaeleza sababu zao za kutumia muziki bandia…kuwa wanaupenda. Hii ni tabia ya kuogofya. Wavuta bangi wanaweza kutetea matumizi yao ya dawa za kulevya kwa maneno hayo hayo, tunaipenda.’ Je, kusema vile kunaweza kuhalalisha matumizi yao? Je, jema na baya‘Muziki umechukua muda ambao ungetumiwa kwa maombi. Muziki ndio kinyago kinachoabudiwa na wengi wa Wakristo watunzao Sabato. Shetani hapingi muziki wowote ikiwa anaweza kupitia hapo kufikia kwenye mawazo ya vijana. Muziki ukitumiwa vibaya huongoza moyo kuwa na kiburi, upuuzi na upumbavu. Muziki kama huo ni laana ya kutisha.’[26]

   ‘Mara nyingi nimeumia moyoni kusikia sauti kali za juu mno zikiharibu maneno matakatifu ya nyimbo za sifa. Sauti kali zinazokwaruza hazifai kabisa katika ibada yenye furaha mbele za . nilitaka kuziba masikio au kukimbia kutoka mahali hapo.’[27]

‘Muziki unaweza kuwa na uwezo mkubwa sana kwa wema ingawa hatutumii uwezo huo wote upasavyo kama sehemu ya ibaada. Mara nyingi uimbaji hutendwa kutokana na hisia au kukidhi malengo maalum na nyakati zingine waimbaji huachwa kusitasita hatimaye muziki huwa na matokeo mabaya katika mawazo ya wasikilizaji. Lakini wakati mwingine huwa vigumu zaidi kudhibiti waimbaji na kuwa fanya wafuate utaratibu kuliko kuboresha mazoea ya maombi. Wengi wa waimbaji hupenda kufanya vitu katika mitindo yao wenyewe, hukataa kushauriwa wala hawavumilii kutawaliwa.’[28]

‘Mazoea mabaya na mwelekeko wa dhambi hutiwa nguvu na kuimarishwa na burudani hizi. Nyimbo za dunia, kuyumbisha sehemu fulani za mwili kunakoashiria hisia za msisimko wa mapenz, maneno na mwelekeo mwovu uaathiri mawazo na kushusha maadili. Kila kijana mwenye mazoea ya kuhudhuria matamasha kama hayo tabia zao huchafuliwa. Katika nchi yetu [Marekani] hakuna kitu kingine chenye mvuto mkubwa kinachotia sumu mawazo yanayoharibu moyo wa kupenda mambo ya kiroho na kupunguza hamu ya utulivu na furaha ya kweli maishani kama tamasha la burudani.’[29]

‘Shetani anaelewa ni kiungo gani cha mwili cha kushitua ili mwili wote usisimke na kuchangamsha akili kisha Kristo hatamaniki tena moyoni.[30]

‘Muziki mbaya hujaa lugha isiyoeleweka na sauti zisizolingana. Mungu hapendezwi na mvurugano.’[31]

‘Nawezaje kuvumilia fikira hii ati “wengi wa vijana wetu wa kizazi hiki hawatafikia uzima wa milele. Oh! Ningalipenda kuwa hizo sauti za vyombo vya muziki zikome ili vijana wasiendelee kutumia muda wa thamani kubwa kwa kujifurahisha tu.[32]

Malaika wanavinjari karibu na nyumba ambamo vijana wanakutana. Kuna mvumo wa sauti za vyombo vya muziki. Wakriso wanakutana pale, lakini unasikia kitu gani pale? Ni nyimbo za pambio za kipuuzi tu zisizositahili kuimbwa katika ukumbi wa ibaada. Tazama malaika watakatifu hukunja mbawa zao karibu nao, ndipo wale walio nyumbani hufunikwa gizani, kasha malaika huondoka pale, nyuso zao zikijaa huzuni, wanalia. Haya niliyaona mara nyingi yakitokea kati ya makundi ya watunzao Sabato.’[33]

Katika uzoefu wa wale ambao maisha yao hutawaliwa na nyimbo za “pop”, “Regge”, nk. Swala la mema na mabaya hufikiriwa juu juu tu.’[34]

‘Muziki mbaya huimbwa na kwaya za kidunia ambazo hutegemea kupata fedha.’[35]

‘Kujionyesha sio dini wala utakaso. Hakuna kinachomchukiza Mungu kulko muziki ambao unaotolewa na vyombo wakati ambapo wanaopiga vyombo hivyo hawakujitoa kamili kwa Mungu.’[36]

‘Mtindo wa mavazi yavutiayo sana, nyimbo zisizo fuata taratibu za maadili ya uimbaji, hazikaribishi kwaya za malaika wa mbinguni makanisani namachini pa Mungu, vitu hivi vyote ni matawi ya mtini usiozaa matunda bali majani mabichi tu.’[37]




[1] Samuele Bacchocch, The Chrsitian and the Rock Music: A Study on Biblical Principles of Music, ‘Biblical Principles of  Music, p. 193.
[2] Samuele Bacchiocchi,  The Christian and the Rock Music: A Study on Biblical Pricinciples of Music, Biblical Pricnicples of Music, pp 194-5 cf. Bible Works; Benjamin Davidson, The Analytical Hebrew and Chaldee Lexcon (Grand Rapids, Michigan: Zondervan Publishing House, 1993), p. 679
[3] Samuelle Bacchiocchi, p. 223.
[4] King James Version, The Study Bible Presenting The Old and The New Testament in the E.G. White Scripture  Comments (Maryland: Review and Herald Publishing Association, 1993), p. 670.
[5] Rosalie H. Zinke, Adult Teachers Sabbath School Bible Study Guide: Worship in the Psalms, Lesson 7, p. 77.
[6] Benjamin Davidson, The Analytical Hebrew and Caldee Lexicon (Grand Rapids, MG: Zondervan Publishing House, 1993), p.394.
[7] Ellen G. White, Selected Messages (3Vols, Washington, D.C.: Review and Herald Publishing Association, 1958), vol. 2, p. 36.
[8] Ellen G. White, Selectd Messages, vol. 2, p. 37, 38.
[9] Ellen G. White, Selected Messages 93vols, Washington, DC: Reviewe and Herald Publishing Association, 1958), vo. 2, pp. 36-37.
[10] Ellen G. White, Selected Messages, vol. 2, p. 37.
[11]Ellen G. White, Testimonies for the Church (9Vools, Cal: Pacific Press Publishing Association, 1948), vol. 1, p.457
[12] Samuele Bacchiocchi,  The Christian and the Rock Music: A Study on Biblical Pricinciples of Music, Biblical Pricnicples of Music, pp 194-5 cf. Bible Works; Benjamin Davidson, The Analytical Hebrew and Chaldee Lexcon (Grand Rapids, Michigan: Zondervan Publishing House, 1993), p. 679
[13] Ellen G. Whtie, Evangelism, p. 505
[14] Samele Bacchiocchi, The Christian and the Rock Music: A Study of Biblical Priinciples of Music, Biblical principles of Music, p. 198.
[15]Samuele Bacchiocchi, The Christian and the Rock Music: A Study on Biblical Principle of Music, Biblical Principles of Music, p. 201-2.
[16] Ellen G. Whtie, Evangelism, p. 505
[17] Samuelle Bacchiocchi,  p. 206
[18]John W. Kleinig, p. 80 (Samuelle Bacchiocchi p. 206).
[19] Samuelle Bacchiocchi, p. 206.
[20] Garen L. Wolf, Music of the Bible in Christian Perspective (Salem, OH, 1996), p. 287 cf. Samuelle Bacchiocchi, p. 207.
[21] Samuelle Bacchocchi, p. 207.
[22] Samuelle Bacchiocchi, p. 208.
[23] Ellen G. White, Testimonies for the Church (9Vols, Cal. : Pacific Press Publishing Association, 19480, VOL. 1, 506.
[24] Ellen G. White, Selected Messages, vol. 2, p. 36.
[25] Ellen G. White, Selected Messages, vol. 2, p. 35.
[26] Ellen G. White, Testimonies for the Church (9vols, ), vol. 1, p. 506.
[27] Ellen G. White, Evangelism, p. 508.
[28] Ellen G. White, Evangelsim, pp 507-8
[29] Ellen G. White, Testimonies for the Church (9vols, ), vol. 4, p. 653.
[30] Ellen G. White, Testimonies for the Church (9 vols,  ), vol. 1, p. 497.
[31] Ellen G. White, Evangelism, p.510.
[32] Ellen G. White, Testimonies for the Church (9vols,  ), vol. 2, p. 144.
[33] Ellen G. White, Messages to Young People, p. 97, 297.
[34] Review and Herald, Decewmber 2, 1972.
[35] Ellen G. White, Evangelism, p. 509.
[36] Ellen G. White, Evangelism, p. 510.
[37] Ellen G. White, Evangelism, p. 511.

No comments:

Post a Comment