Waweza Kuishi na Yesu, lakini huwezi kuishi bila Yesu.Yohan 3:16


TWAWEZA KUIAMINI BIBLIA
Mabaharia waasi maarufu walioizamisha meli ya Kiingereza iliyoitwa Bounty waliishia kufanya makazi yao wakiwa pamoja na wanawake, wenyeji wa eneo lile katika kisiwa cha Pitcairn katika Bahari ya Pasifiki ya Kusini. Kundi lile lilikuwa mabaharia tisa wa Kiingereza, wanaume wa Kitahiti sita, wanawake wa Kitahiti kumi, na msichana wa miaka kumi na mitano. Mmojawapo wa mabaharia wale alivumbua namna ya kutonesha [kugeuza kuwa mvuke] alkoholi, na baada ya muda mfupi ulevi ukaliharibu koloni lile lililokuwa katika kisiwa kile. Ugomvi kati ya wanaume na wanawake ukageuka na kuwa wa kutumia nguvu.
Baada ya kupita muda fulani mmoja tu kati ya wanaume wale wa kwanza waliofika mle kisiwani ndiye alibaki kuwa hai. Lakini mtu huyo, Alexander Smith, alikuwa ameigundua Biblia katika mojawapo la makasha yaliyochukuliwa kutoka katika ile meli. Alianza kuisoma na kuwafundisha wengine juu ya kile ilichosema. Alipofanya hivyo maisha yake yeye mwenyewe yakabadilika na hatimaye maisha ya wote waliokuwa katika kisiwa kile.
Wakazi wa kisiwa kile walikuwa wametengwa na ulimwengu wa nje mpaka ilipowasili meli ya Kimarekani iliyoitwa Topaz katika mwaka wa 1808. Wafanyakazi katika meli hiyo wakakikuta kisiwa kile kikiwa na jumuia inayokua na kusitawi, bila ya kuwa na pombe kali (wiski), gereza, wala uhalifu. Biblia ilikuwa imekigeuza kisiwa kile kutoka jehanamu ya duniani kwenda katika kielelezo cha vile Mungu atakavyo ulimwengu huu uwe. Na mpaka leo hii kinaendelea kuwa katika hali hiyo.
Je, hivi Mungu bado anaendelea kusema na watu kupitia katika kurasa hizo za Biblia? Bila shaka anafanya hivyo. Ninapoandika haya, naliangalia karatasi la majibu lililotumwa kwetu na mwanafunzi mmojawapo wa kozi zetu za Biblia. Maelezo chini yake yanasema hivi "Mimi nimo gerezani, niko katika orodha ya watu wanaostahili kunyongwa, nimehukumiwa kufa kwa kutenda kosa la jinai. Kabla ya kuchukua kozi hii ya Biblia, nilikuwa nimepotea lakini sasa ninacho kitu cha kutumainia tena nimeupata upendo mpya."
Biblia inao uwezo unaoweza kuyabadilisha kabisa maisha ya watu. Kwa kweli, watu wanapoanza kujifunza Biblia, maisha yao hubadilika kwa namna ya kuvutia sana.

1. Jinsi Mungu Anavyozungumza Nasi Kupitia Katika Biblia

Baada ya kumwumba Adamu na Hawa, yaani, yule mwanaume na mwanamke wa kwanza wa duniani, Mungu alizungumza nao uso kwa uso. Lakini Mungu alipokuja kuwatembelea baada ya wao kutenda dhambi, je, wale watu wawili walifanya nini?
"Mwanaume yule na mkewe wakasikia sauti ya BWANA Mungu alipokuwa akitembea mle bustanini wakati wa jua kupunga, nao WAKAJIFICHA ASIWAONE BWANA MUNGU katikati ya miti ya bustani." (Mwanza 3:8). 
Dhambi ilikata mawasiliano ya ana kwa ana kati ya mwanadamu na Mungu. Baada ya dhambi kuingia katika ulimwengu huu, je, Mungu aliwasilianaje na watu?
"Hakika Bwana Mwenyezi hafanyi kitu, bila kuwafunulia watumishi wake manabii nia yake." - Amosi 3:7.
Mungu hakutuacha sisi gizani kuhusu maisha haya tuliyo nayo na maana yake. Kupitia kwa manabii wake - yaani, watu wale aliowaita Mungu kuwa wanenaji na waandishi wake - wamefunua majibu yake kwa maswali makuu yahusuyo maisha yetu.

2. Ni Nani Aliyeiandika Biblia?

Manabii waliutoa ujumbe wa Mungu kwa kutumia sauti na kalamu zao katika kipindi chao walichoishi, na walipokufa, maandiko yao yaliendelea kuwapo baada yao. Kisha ujumbe huo wa manabii ulikusanywa pamoja chini ya uongozi wake Mungu, na kuwekwa katika kitabu tunachokiita Biblia.
Lakini maandiko yao hayo yanaaminika kwa kiasi gani?
"Zaidi ya hayo, lakini kumbukeni kwamba hakuna mtu ye yote awezaye kufafanua mwenyewe unabii ulio katika Maandiko Matakatifu. Maana hakuna ujumbe wa kiunabii unaotokana na matakwa ya binadamu bali watu walitoa unabii wakiongozwa na Roho Mtakatifu" (2 Petro 1:20,21).
Waandishi wa Biblia waliandika si kwa kufuata mapenzi au tamaa yao, bali kama walivyoongozwa au kuvuviwa na Roho wa Mungu. Biblia ni kitabu cha Mungu!
Katika Biblia hiyo Mungu hutuambia habari zake Mwenyewe, tena hutufunulia makusudi yake aliyo nayo kwa ajili ya wanadamu. Inaonyesha mtazamo wa Mungu kwa mambo yale yaliyopita, kisha inatufunulia mambo ya mbele, ikitueleza jinsi tatizo la uovu litakavyotatuliwa mwishoni na jinsi amani itakavyokuja katika dunia yetu.
Je, hivi Biblia yote ni ujumbe utokao kwa Mungu?
"Maandiko yote, Matakatifu yameandikwa kwa uongozi wa Mungu, na yanafaa kuonya, kusahihisha makosa yao, na kuwaongoza, katika kufundishia ukweli, mtu wa Mungu awe mkamilifu na tayari kabisa kufanya kila kazi njema, waishi maisha adilifu" - (2 Timotheo 3:16,17).
Biblia Takatifu huyabadilisha kabisa maisha ya wanadamu kwa sababu Biblia "yote" ina "pumzi ya Mungu," ni hati iliyovuviwa, ni kitabu cha Mungu. Manabii walisimulia kile walichokiona na kukisikia kwa kutumia lugha ya wanadamu, lakini ujumbe wao ulitoka moja kwa moja kwa Mungu. Kwa hiyo, ukitaka kujua maisha haya yana maana gani, soma Maandiko Matakatifu. Kuisoma Biblia kutayabadilisha kabisa maisha yako. Kadiri unavyozidi kuisoma kwa maombi, ndivyo utakavyozidi kupata amani moyoni mwako.
Roho Mtakatifu yule yule aliyewavuvia manabii kuandika, Biblia hiyo, atayafanya mafundisho ya Biblia, injili yake, ifae kuyabadilisha kabisa maisha yako ukimwalika Roho kuwapo wakati unapoisoma hiyo Biblia.

3. Umoja wa Biblia

Kwa kweli Biblia ni maktaba ya vitabu 66. vitabu 39 vya Agano la Kale viliandikwa kuanzia karibu na mwaka wa 1450 K.K hadi 400 K.K, Vitabu 27 vya Agano Jipya viliandikwa kati ya mwaka wa 50 B.K na mwaka wa 100 B.K.
Nabii Musa alianza kuandika vitabu vitano vya kwanza wakati fulani kabla ya mwaka wa 1400 K.K. Mtume Yohana alikiandika kitabu cha mwisho cha Biblia, yaani, kitabu cha Ufunuo, karibu na mwaka wa 95 B.K. Katika kipindi cha miaka 1,500 kati ya kuandikwa kitabu cha kwanza na cha mwisho cha Biblia, walau watu wengine wapatao 38 waliovuviwa walitoa mchango wao. Wengine walikuwa wafanya biashara, wengine wachungaji wa kondoo, wengine wavuvi, wengine askari, matabibu, wahubiri, wafalme - wanadamu toka katika tabaka zote za maisha. Mara nyingi waliishi katika utamaduni na falsafa vilivyohitilafiana.
Lakini hapa ndipo yalipo maajabu ya maajabu yote: Vitabu hivyo 66 vya Biblia pamoja na sura zake 1,189 zenye idadi ya mafungu 31,173 vikiwekwa pamoja, tunaona umoja na mwafaka katika ujumbe vinaoutoa.
Hebu na tuseme kwamba mtu mmoja anagonga mlangoni pako, halafu anapokaribishwa ndani, anaweka kipande cha marumaru chenye umbo la ajabu juu ya sakafu ya chumba chako cha kuongea, halafu anaondoka bila kusema neno lo lote. Wageni wengine wanamfuata, mmoja baada ya mwingine, mpaka takribani watu 40 wanaweka kila mmoja kipande chake cha marumaru mahali pake.
Wa mwisho anapokwenda zake, kwa mshangao wewe unaona jengo zuri limesimama mbele yako. Ndipo wewe unajifunza kwamba sehemu kubwa ya "mafundi hao wanachonga mawe" hawajawahi kuonana kamwe, wakiwa wamekuja, kama walivyofanya, kutoka Amerika ya Kusini, China, Urusi, Afrika na sehemu nyingine za ulimwengu.
Je, wewe ungeamua nini? Ya kwamba mtu fulani alipanga umbo hilo lililojengwa kwa mawe ya kuchonga naye alimtumia kila mtu vipimo sahihi kutokana na kipande chake kile kimoja cha marumaru.
Biblia nzima inatoa ujumbe mmoja unaoshikamana - sawasawa tu na lile jengo la mawe yaliyochongwa ya marumaru. Mtu fulani mmoja mwenye akili alipanga yote hayo, yaani, ni akili za Mungu. Umoja wa kushangaza wa Maandiko Matakatifu unatoa ushahidi wake kwamba ingawa ni wanadamu walioyaandika mawazo yale, yalikuwa yamevuviwa naMungu.

4. Waweza Kuiamini Biblia

1. Kuhifadhiwa kwa Biblia ni jambo la ajabu sana. Maandiko yote ya awali ya Biblia yalinukuliwa kwa mkono - muda mrefu kabla ya kuwako
mitambo ya kuchapisha vitabu. Waandishi wale walitayarisha nakala za maandiko ya mkono ya asilia na kuzitawanya. Maelfu ya nakala kama hizo za maandiko ya mkono au sehemu zake bado ziko mpaka sasa.
Maandiko ya mkono ya Kiebrania yanayorudi nyuma hadi ule mwaka wa 150 mpaka 200 kabla ya Kristo yalipatikana karibu na Bahari ya Chumvi mnamo mwaka 1947. Ni jambo la kushangaza sana kwamba magombo hayo mawili yenye umri wa miaka elfu mbili yanazo kweli zile zile tunazozikuta katika Agano la Kale la Biblia zinazochapishwa siku hizi. Huu ni ushahidi wenye nguvu unaoonyesha jinsi Neno la Mungu linavyoaminika.
Mitume waliandika kwanza sehemu kubwa ya Agano Jipya kama nyaraka walizozituma kwa makanisa ya Kikristo yaliyoanzishwa baada ya kifo na ufufuo wake Kristo. Zaidi ya maandiko ya mkono 4,500 ya Agano Jipya lote au sehemu yake yanapatikana katika nyumba za Makumbusho na maktaba za Ulaya na Amerika. Baadhi yake yanakwenda nyuma hadi karne ile ya pili. Kuyalinganisha maandiko hayo ya mkono ya awali na biblia ya siku hizi, twaweza kuona kwa urahisi kwamba kwa kawaida Agano Jipya limeendelea pia kubaki bila mabadiliko yo yote tangu lilipoandikwa kwa mara ya kwanza.
Siku hizi Biblia au sehemu zake zimetafsiriwa katika lugha zaidi ya 2,060 na (dialects). Ni kitabu kinachouzwa sana ulimwengu: zaidi ya Biblia milioni 150 na sehemu za Biblia huuzwa kila mwaka.
2. Usahihi wa Biblia kihistoria ni wa kushangaza sana. Uvumbuzi mwingi wa elimu ya mambo ya kale (akiolojia) umethibitisha kwa namna ya kuvutia sana usahihi wa Biblia. Wanahistoria wamevigundua vibao vya udongo wa mfinyanzi pamoja na majengo ya kumbukumbu ya mawe ambayo yameonyesha majina, mahali, na matukio yaliyojulikana kuhusu siku za nyuma kutokana na Biblia tu.
Kwa mfano, kulingana na Mwanzo 11:31, Ibrahimu na familia yake "wakatoka wote katika Uru... waende katika nchi ya Kanaani." Kwa kuwa ni Biblia peke yake iliyosema juu ya Uru, mabingwa fulani wa Biblia walisema kwamba mji kama huo ulikuwa haujapata kuwako kamwe. Ndipo wachimbaji wa mambo ya kale wakagundua mnara wa hekalu katika nchi ya Iraki Kusini ukiwa na kwenye msingi wake iliyoandikwa katika maandishi ya kikabari yaliyokuwa na jina la Uru. Ugunduzi wa baadaye ulionyesha kwamba Uru ulikuwa ni mji mkuu ambao ulikuwa unasitawi wenye ustaarabu wa hali ya juu uliokuwa umefikiwa. Sura ya mji ule ilikuwa imesahaulika ni Biblia peke yake iliyolihifadhi jina lake - mpaka pale koleo ya mwanaakiolojia mmoja ilipouthibitisha ukweli wa kuwako kwake. Na huo Uru ni mmoja tu miongoni mwa mifano mingi ya akiolojia inavyothibitisha usahihi wa Biblia.
3. Kutimia kwa usahihi kabisa kwa utabiri wa Biblia hukuonyesha wewe kwamba unaweza kuitegemea Biblia. Maandiko hayo yana utabiri mwingi wa kushangaza sana wa matukio ya siku za usomi ambayo hivi sasa yanaendelea kutimia mbele ya macho yetu. Tutauchunguza baadhi ya unabii huo wa kusisimua katika masomo ya mbele.

5. Jinsi Ya Kuielewa Biblia

Unapolichunguza Neno la Mungu, weka kanuni hizi mawazoni mwako:
1. Jifunze Biblia ukiwa na moyo wa maombi. Ukiyaendea Maandiko Matakatifu kwa moyo na mawazo yaliyofunguliwa kwa maombi, yatageuka na kuwa mawasiliano kati yako na Yesu (Yohana 16:13-14).
2. Soma Biblia kila siku. Kujifunza Biblia kila siku ni ufunguo wa kupata nguvu katika maisha yetu, ni kukutana na mawazo ya Mungu (Warumi 1:16).
3. Unapoisoma, iache Biblia ijieleze yenyewe. Uliza: mwandishi huyu wa Biblia alikusudia kusema nini? Kwa kuzingatia kile limaanishacho fungu hilo, twaweza kuitumia kwa akili katika maisha yetu ya leo hii.
4. Soma Biblia kwa kufuata somo. Linganisha andiko na andiko. Yesu alitumia mbinu hii kuthibitisha kwamba yeye alikuwa ndiye Masihi:
"Akaanza kutoka Musa na Manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe."
5. Jifunze Biblia ili kupokea uwezo wa kuishi kwa ajili ya Kristo. Neno la Mungu limeelezwa katika Waebrania 4:12 kama upanga mkali ukatao kuwili. Ni zaidi ya maneno tu yaliyo juu ya ukurasa, ni silaha iliyo hai mikononi mwetu ya kupigia na kuyaondolea mbali majaribu yale yanayotushawishi kutenda dhambi.
6. Sikiliza Mungu anapozungumza nawe kupitia katika Neno lake. Endapo mtu anataka kuujua ukweli wa Bilbia juu ya somo fulani, basi, ni lazima awe tayari kufuata yale inayofundisha (Yohana 7:17), sio yale anayofikiri mtu fulani, au yale yanayokaziwa na fundisho lolote la kanisa lake.

6. Biblia Yaweza Kubadilisha Maisha Yako

"Kuyafafanua maneno yako [Mungu] kwatia nuru, kunampa ufahamu mjinga" - (Zaburi 119:130).
Kujifunza Biblia kutauimarisha "ufahamu" wako, kutakupa nguvu ya kuyashinda mazoea yale yaletayo madhara, na kukuwezesha kukua kimwili, kiakili, kimaadili na kiroho.
Biblia inazungumza na moyo. Inashughulika na mambo yale yanayowapata wanadamu katika maisha yao - yaani, upendo, ndoa, uzazi na kifo. Inaliponya jeraha lenye kina kirefu sana katika tabia ya mwanadamu, pamoja na dhambi na taabu inayotokana nayo.
Neno la Mungu si kitabu cha jamii moja, kizazi kimoja, taifa moja, au utamaduni mmoja. Japokuwa liliandikwa katika nchi ya Masharikiya kati, linawavutia pia wanaume na wanawake wa Magharibi. Linaingia katika nyumba za wanyonge na katika majumba makubwa ya matajiri. Watoto wanazipenda hadithi zake zinazosisimua. Mashujaa wake wanawavutia sana vijana. Wagonjwa, wanaoishi katika hali ya upweke, na wazee wanagundua ndani yake faraja na tumaini la kuwa na maisha bora.
Kwa kuwa Mungu anafanya kazi yake kupitia katika Biblia, basi, inao uwezo mkubwa. Inaivunjavunja hata mioyo iliyofanywa migumu dhidi ya hisia zote za kibinadamu, inailainisha na kuijaza na upendo. Tumeona Biblia ikimbadilisha haramia wa zamani na mvuta bangi na kumfanya mhubiri aliye motomoto. Tumeona Biblia ikimbadilisha mwongo na mdanganyaji na kumfanya kuwa mwalimu mwaminifu na mwenye kuheshimika. Tumeona kitabu hicho kikiwanyakua watu wakiwa karibu na kujiua wenyewe na kuwapa tumaini la kuanza maisha upya. Biblia inaamsha upendo miongoni mwa maadui. Inawafanya wenye majivuno kuwa wanyenyekevu, na wachoyo kuwa wakarimu. Biblia inatutia nguvu tunapokuwa dhaifu, inatuchangamsha tunapokuwa katika hali ya kukata tamaa, inatufariji tunapokuwa na huzuni, inatuongoza tunapochoka sana. Inatuonyesha jinsi ya kuishi kwa ujasiri na jinsi ya kufa bila hofu.
Kitabu hicho cha Mungu, yaani, Biblia kinaweza kuyabadilisha maisha yako! Utagundua hivyo kwa dhahiri zaidi na zaidi, kadiri unavyoendelea kujifunza miongozo hii ya GUNDUA.
Kwa nini Biblia hiyo iliandikwa kwa ajili yetu? Yesu anatoa jibu: "Lakini hizi [kweli za Biblia] zimeandikwa; ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini muwe na uzima kwa jina lake" - (Yohana 20:31).
Sababu kuu kuliko zote kwa nini sisi tunapaswa kuyafahamu Maandiko Matakatifu ni kwamba yamejaa picha zinazomfunua Yesu Kristo na kutuhakikishia sisi uzima wa milele. Kwa kumtazama Kristo katika Biblia nzima, tunabadilika na kufanana naye zaidi. Basi, kwa nini wewe usianze sasa kugundua uwezo huo wa Neno la Mungu uwezao kukufanya wewe kufanana zaidi na Yesu?

YACHUNGUZENI MAANDIKO

TWAWEZA KUMWAMINI MUNGU
Siku moja Jimi alimwuliza mtu mmoja anayekana kuwa kuna Mungu endapo alipata kujaribu sana, hata kwa dakika chache tu, kupigana na wazo lisemalo kwamba huenda Mungu yuko.
"Sawa kabisa!" mkana Mungu yule akajibu, akimwacha Jimi na mshangao. "Miaka mingi iliyopita, mimi nilikuwa karibu sana nigeuke na kuwa mtu anayemwamini Mungu. Nilipokiangalia kile kiumbe kidogo sana - lakini - kikamilifu katika kitanda chake kidogo, nilipochungulia na kuviona vidole vile vidogo fahamu za kwanza za kutambua, nilipita katika kipindi cha miezi kadhaa ambayo katika hiyo mimi nilikuwa karibu kabisa niache kuwa mkana Mungu. Kule kumwangalia mtoto yule kulikuwa kumenishawishi karibu kabisa kuwa hapana budi Mungu alikuwa yuko."
1. Kila Kitu Kilichobuniwa Kina Mbunifu Wake
Muundo wa mwili wa kibinadamu unafanya iwepo haja ya kuwako mbunifu wake. Wanasayansi wanatuambia kwamba ubongo wetu hukusanya na kukumbuka picha elfu nyingi katika mawazo yetu, huyaunganisha matatizo yetu yote na kuyatatua, hufurahia kuona uzuri, huitambua nafasi ya mtu, na kutaka kukuza yaliyo bora ndani ya kila mtu. Chaji za umeme zitokazo katika ubongo huongoza shughuli zote za misuli ya miili yetu.
Kompyuta pia zinafanya kazi kwa njia ya mikondo ya umeme. Lakini ilichukua akili ya mwanadamu katika kuitengeneza hiyo kompyuta na kuiambia la kufanya.
Si ajabu, basi, kwamba mtunzi wa Zaburi alihitimisha kwa kusema kwamba mwili wa mwanadamu unasimulia habari za Muumbaji huyo wa ajabu kwa sauti kubwa iliyo wazi:
"Nakusifu maana nimefanywa kwa namna ya ajabu, matendo yako ni ya ajabu, wewe wanijua kabisa kabisa" - (Zaburi 139:14)

Hatuna haja ya kwenda mbali ili kuyaona hayo "matendo" ya Mungu. Umbo la ubongo wetu wenye sehemu nyingi za ajabu na viungo vyetu vingine ni "matendo" ya Mungu, nayo husonda kidole chake kwa yule mbunifu stadi kabisa.
Hakuna pampu yoyote iliyotengenezwa na mwanadamu inayoweza kulinganishwa na moyo wa mwanadamu. Hakuna mtandao wo wote wa kompyuta uwezao kuwa sawa na mfumo wetu wa mishipa ya fahamu. Hakuna mfumo wo wote wa Televisheni unaofanya kazi yake vizuri kama sauti, sikio, na jicho la mwanadamu. Hakuna kiyoyozi kikuu cho chote (central air conditioning) wala mfumo wa kuipasha joto nyumba uwezao kushindana na kazi inayofanywa na pua, mapafu, na ngozi yetu. Mfumo wenye sehemu nyingi za ajabu wa mwili wa mwanadamu unadokeza kwamba mtu fulani alihusika katika kuubuni, na Mtu huyo fulani ni Mungu.
Mwili wa mwanadamu ni mfumo kamili wa viungo mbali mbali - vyote vikiwa vinashirikiana, vyote vikiwa vimeumbwa kikamifu. Mapafu na moyo, mishipa ya fahamu na misuli, hiyo yote hufanya kazi za ajabu mno kiasi cha kuwa vigumu kusadikika ambazo hutegemezwa juu ya kazi nyingine zilizo za ajabu mno kiasi cha kutufanya sisi tushindwe kusadiki.
Endapo ungetakiwa kuzipa nambari sarafu kumi kuanzia moja mpaka kumi, na kuziweka mfukoni mwako, na kuzitikisa-tikisa huku na huku, kisha kuzitoa mfukoni mwako na kuziweka tena mfukoni moja moja, je, kuna uwezekano gani kwamba ungefanya hivyo kwa kufuata mfuatano wa nambari zake sawa sawa? Kwa sheria ya mahesabu unayo bahati moja tu katika bilioni kumi ya kuzitoa kwa mpangilio wake kuanzia ya kwanza mpaka ile ya kumi.
Sasa, basi, hebu fikiria ni bahati ngapi tumbo la chakula, ubongo, moyo, ini, arteri, vena, figo, masikio, macho, na meno vingekuwa nazo vikikua vyote pamoja na kuanza kufanya kazi yao kwa dakika ile ile ya wakati mmoja.
Hivi maelezo ya busara kabisa ni yapi kuhusu ubunifu huo wa mwili wa mwanadamu?
"Kisha Mungu akasema, 'Natumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu,'..............Hivyo Mungu Akamwuumba Mtu Kwa Mfano Wake,...... mwanamume na mwanamke aliwaumba" - (Mwanzo 1:26,27).
Mwanaume na mwanamke wa kwanza wasingeweza kuwa wametokea wenyewe tu. Biblia inathibisha kwamba Mungu alitubuni sisi kwa mfano wake. Alituwaza katika mawazo yake na kutuumba.
2. Kila Kitu Kilichoumbwa Kina Muumbaji Wake
Lakini ushahidi wa kuwako kwake Mungu haufungamani tu na ubunifu wa miili yetu; pia umetandaa huko mbinguni. Acha taa za mjini, angalia juu katika mbingu ya usiku. Wingu lile jeupe kama maziwa lenye nyota, tunaloliita Mkanda wa Nuru (Milky Way) ambalo kwa kweli ni kundi la mabilioni ya majua (galaxy) yanayotoa mwanga mkali wa moto sawa na ule wa jua letu ambao unaweza kuonekana hapa duniani kwa kupitia katika darubini kubwa zilizopo hapa duniani kama ile darubini iitwayo "Hubble Telescope" iliyo katika anga za juu.
Si ajabu, basi, kwamba mtunga Zaburi alihitimisha kwa kusema kwamba nyota zinamtangaza Muumbaji Mtukufu:
"Mbingu zatangaza utukufu wa Mungu, anga ladhihirisha kazi ya mikono yake" (Zaburi 19:1-3).
Je, hivi sisi twaweza kutoa hitimisho gani la busara kwa kuangalia mpangilio huo unaotatanisha sana na ukubwa wa malimwengu yote?
"Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi" (Mwanzo 1:1).
"Yeye [Mungu] alikuwako kabla ya vitu vyote; vyote hudumu mahali pale kwa uwezo wake" (Wakolosai 1:17).
Viumbe vyote humshuhudia yule Mungu Mbunifu Mkuu na Muumbaji asiye na Mwisho. Katika maneno haya rahisi, "Hapo mwanzo Mungu," tunalipata jibu la siri ile ya uhai. Yuko Mungu aliyeumba kila kitu.
Wanasayansi wakuu wengi siku hizi wanamwamini Mungu. Dk. Arthur Compton, mwanafizikia mshindi wa tuzo ya Nobel, akitoa maoni yake juu ya fungu hilo la Maandiko, siku moja alisema hivi:
"Kwangu binafsi, imani huanza ninapotambua kwamba yule aliye na akili isiyo na kifani ndiye aliyeyaweka hayo malimwengu na kumwumba mwanadamu. Kwangu mimi si vigumu kuwa na imani hii, kwa maana ni dhahiri kwamba po pote pale palipo na mpango yupo Mungu mwenye akili. Malimwengu yaendayo kwa utaratibu, na kujifunua kwetu hushuhudia ukweli wa usemi huu adimu mno uliopata kunenwa - 'Hapo mwanzo Mungu'"
Biblia haijaribu kumthibitisha Mungu inatangaza kuwako kwake. Dk. Arthur Conklin, mwana biolojia, siku moja aliandika hivi: "uwezekano kwa uhai kutokea kwa ajali ni sawa na uwezekano kwa kamusi kamili kutokea kutokana na mlipuko katika kiwanda cha kuchapisha vitabu".
Twajua kwamba wanadamu hawawezi kutengeneza kitu cho chote bila kutumia kitu kingine. Twaweza kujenga vitu, kuvumbua vitu, kuunganisha vitu, lakini kamwe hatujapata kufanya kitu cho chote bila kuwa na kitu kingine cha kuanzia, awe ni chura mdogo kabisa ua la kawaida kabisa. Vitu vituzungukavyo pande zote hupiga kelele vikisema Mungu ndiye aliyevibuni, Mungu ndiye aliyeviumba, Mungu ndiye anayevitegemeza. Jibu pekee linaloaminika kuhusu chimbuko la malimwengu hayo, dunia hii, na wanadamu - ni Mungu.
3. Mungu Huingia Katika Mahusiano Na Watu Binafsi
Mungu yule aliyezibuni mbingu hizo na nyota, aliyeyaumba malimwengu hayo, anatafuta kuwa na uhusiano nasi binafsi. Alikuwa na uhusiano wake binafsi na Musa: "Bwana akasema na Musa....kama vile mtu asemavyo na rafiki yake" (Kutoka 33:11). Mungu Mwenyewe anataka kuingia katika uhusiano nawe na kuwa Rafiki yako. Yesu aliwaahidi wale wanaomfuata, akisema "Ninyi mmekuwa rafiki zangu" (Yohana 15:14).
Sisi sote tumeshughulika sana na wazo hilo la Mungu, kwa kuwa wanadamu kwa asili wanapenda dini. Hakuna mnyama yeyote ajengaye madhabahu kwa ajili ya ibada. Lakini kila mahali unapowakuta wanaume na wanawake, unawakuta wakiabudu. Ndani ya kila moyo wa mwanadamu kuna ufahamu kuwa Mungu yuko, tamaa ya kuwa rafiki wa Mungu. Tunapoitikia hiyo tamaa yetu na kumpata Mungu, hatuwi na mashaka tena juu ya kuwako kwake na hitaji letu.

Katika miaka ile ya 1990 mamilioni ya wanaomkana Mungu katika nchi ya Urusi waliachana na imani yao hiyo ya kumkana Mungu, kisha wakamgeukia Mungu. Profesa wa Chuo Kikuu cha St. Petersburg alitoa kauli yake inayofanana na maoni yaliyotolewa na wakana Mungu wengi katika Umoja wa Kisovieti iliyopita:
"Nimetafuta maana ya maisha katika utafiti wangu wa kisayansi, lakini sikuona kitu chochote cha kutegemea. Wanasayansi wanaonizunguka mimi wanazo hisia hizo hizo za ukiwa. Nilipoangalia ukubwa wa malimwengu katika somo langu la elimu ya nyota, kisha nikaangalia ukiwa uliomo moyoni mwangu, niliona kwamba ni lazima pawe na maana fulani. Kisha nilipoipokea Biblia uliyonipa na kuanza kuisoma, ukiwa katika maisha yangu ukajazwa. Nimeiona Biblia kuwa ndiyo chimbuko la pekee la matumaini kwa nafsi yangu. Nimempokea Yesu kama Mwokozi wangu, nami nimepata amani ya kweli pamoja na kuridhika katika maisha yangu".
Mkristo anamwamini Mungu kwa sababu yeye amekutana naye na kugundua kwamba anayatosheleza mahitaji makubwa sana ya moyo wake. Mungu ambaye Wakristo wamemuona kuwa yuko, anatupatia mtazamo mpya, maana mpya, makusudi mapya na furaha mpya.
Mungu hatuahidi sisi kwamba tutakuwa na maisha yasiyo na taabu, wala mapambano, ila yeye anatuhakikishia kwamba atatuongoza na kutusaidia kama tutakuwa na uhusiano binafsi naye. Na mamilioni ya Wakristo wanaweza kutoa ushuhuda wao kwamba ingekuwa heri kwao kuacha kila kitu kuliko kuyarudia maisha yale yasiyokuwa na Mungu.
Hii ndiyo ajabu kuu kuliko zote kwamba yule Mungu Mwenyezi aliyeyabuni, aliyeyaumba na kuyategemeza malimwengu hayo anataka kufanya uhusiano na kila mwanaume na mwanamke, kila mvulana na msichana. Daudi alishangaa sana kuhusu jambo hilo alipoandika maneno haya:
"Nikiangalia mbingu, kazi ya vidole vyako, mwezi na nyota ulizozimika huko, mtu ni nini ee Mungu hata umfikirie mwanadamu ni nini hata umjali?" - (Zaburi 8:3,4).
Muumbaji wetu ana "mjali" kila mmoja wetu. Yeye binafsi anakupenda sana wewe kana kwamba wewe ulikuwa ni kiumbe chake cha pekee alichokiumba.
Basi tunaweza kumwamini Mungu:
(1) Kwa sababu ya ubunifu wake wenye sehemu nyingi katika kila kitu alichokiumba ambacho kinatuzunguka sisi.
(2) Kwa sababu shauku ile iliyomo ndani yetu juu ya Mungu inatufanya tusiwe na raha mpaka tupatapo pumziko letu ndani yake tena.
(3) Kwa sababu tunapomtafuta na kumpata, Mungu hutosheleza kila haja tuliyo nayo pamoja na shauku yetu - kikamilifu!

4. Ni Mungu Wa Aina Gani?
Ni jambo la busara tu kwamba Mungu aliye na nafsi yake apende kujifunua mwenyewe kwa viumbe wake kama vile baba atakavyo watoto wake wamjue. Na katika Biblia Mungu anatuambia yeye ni nani, tena anafananaje.
Ni mfano gani alioutumia Mungu katika kuwaumba wanaume na wanawake?
"Hivyo Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba" (Mwanzo 1:27).
Kwa kuwa sisi tumeumbwa kwa mfano wa Mungu, basi, uwezo wetu wa kufikiri na kujisikia, kukumbuka na kutumaini, kutafakari na kuchambua mambo - chimbuko lake lote latoka kwake. Je, tabia kuu ya Mungu ni ipi?
"Mungu ni upendo" (1 Yohana 4:8).
Mungu hufanya uhusiano wake na wanadamu kutokana na moyo wake wa upendo. Hakuna kitu cho chote alichofanya au atakachopata kufanya ambacho hakijasababishwa na upendo wake usio na ubinafsi, ujitoao mhanga.
5. Jinsi Yesu Anavyotufunulia Alivyo Mungu
Katika Biblia Mungu anarudia tena na tena kueleza habari zake Mwenyewe kwamba Yeye ni Baba.
"Je! Sisi sote si watoto wa baba mmoja"?
"Je, sisi sote hatukuumbwa na Mungu yule yule?" Malaki 2:10.
Baadhi ya mababa tuwaonao leo si cho chote, bali hawapendezi. Kuna mababa wasiojali, mababa wanaotukana matusi. Mungu si kama hao. Yeye anajali, ni Baba anayeguswa sana na mambo yetu. Ni Baba apendaye kucheza na mwanawe au binti yake, ni Baba anayewafurahisha sana watoto wake kwa kuwasimulia hadithi kabla hawajaenda kulala usiku.
Baba yetu huyo mwenye upendo alitaka kufanya zaidi ya kule kujifunua Mwenyewe kwa njia ya maneno ya Maandiko. Alijua kwamba yule mtu tunayeishi naye ni mtu halisi kuliko yule tunayesikia tu habari zake au tunayesoma habari zake. Kwa hiyo yeye akaja katika dunia yetu kama mtu halisi - yaani, yule mtu Yesu.
"Kristo mfano wa Mungu asiyeonekana" - (Wakolosai 1:15).
Basi kama wewe umemwona Yesu, utakuwa umemwona Mungu. Alijishusha hadhi yake na kuwa sawa sawa na sisi akawa kama sisi - ili apate kutufundisha jinsi ya kuishi na kuwa na furaha, ili kwamba sisi tupate kuona jinsi Mungu alivyo hasa. Yesu ni Mungu aliyeonekana kwa macho. Yeye mwenyewe alisema, "Aliyeniona mimi amemwona Baba" (Yohana 14:9).
Usomapo kisa cha Yesu katika vitabu vinne vya Injili, yaani, vitabu vinne vya kwanza vya Agano Jipya, utagundua picha ya kuvutia sana ya Baba yetu aliye mbinguni. Wavuvi wale wa kawaida tu walizitupa nyavu zao ili kumfuata Yesu, na watoto wadogo wakasongamana kwenda kwake kupokea baraka zake. Aliweza, kumfariji mwenye dhambi aliyeharibika kabisa na kuzivunja nguvu za mnafiki sugu aliyejihesabia haki yeye mwenyewe. Aliponya kila maradhi kuanzia upofu hadi ukoma. Katika matendo yake yote Yesu alidhihirisha kwamba Mungu ni upendo! Alikidhi haja ya mwanadamu kwa namna ambayo hakuna mtu ye yote aliyepata kufanya hivyo kabla yake au tangu wakati wake!
Ufunuo wa Yesu wa mwisho ambao unaonyesha utukufu wa jinsi Mungu alivyo ulitokea pale msalabani.
"Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele" - (Yohana 3:16).
Yesu alikufa sio tu kutupatia maisha yenye furaha sasa, bali kutupa uzima wa milele pia. Kwa vipindi virefu watu walishangaa, na kutumaini, na kuota
ndoto juu ya Mungu. Waliiona kazi ya mikono yake mbinguni na katika uzuri wa viumbe vya asili. Kisha pale msalabani, Yesu alikivunjilia mbali kimya cha vizazi vingi, na watu wakajikuta wanautazama ana kwa ana uso wa Mungu, wakimwona yeye kama alivyo hasa - yeye ni upendo, wa milele, tena ni upendo udumuo milele!
Wewe waweza kumgundua Mungu sasa hivi Yesu anapomfunua kwako. Ugunduzi huo utakufanya utoe uthibitisho wako binafsi, ukisema: "Baba, nakupenda!"